Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda akiwasisitizia wahitimu na wageni (hawako pichani) waliofika katika mahafali ya kwanza na ya pili ya Chuo cha Ufugaji Nyuki Tabora kuwa serikali lazima ijenge Chuo KIkubwa Cha Ufugaji Nyuki Tabora.
SERIKALI imeahidi kujenga chuo kikubwa cha mafunzo ya ufugaji nyuki katika eneo la Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki mkoani Tabora ili kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya kwanza Barani Afrika katika uzalishaji wa mazao yatokanayo na nyuki.SERIKALI KUJENGA CHUO KIKUBWA CHA MAFUNZO YA UFUGAJI NYUKI NCHINI
Written By Sema Naye - Naipenda Tanzania on Saturday, August 31, 2013 | 9:50 PM
Ahadi hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda aliyekuwa Mgeni Rasmi katika mahafali ya kwanza na ya pili ya Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji nyuki Tabora alipokuwa akiwahutubia wahitimu kabla ya kuwatunuku vyeti na zawadi.
Mhe. Pinda alisema pamoja na mapungufu ya chuo hicho yaliyotokana na tabia ya kuhamisha mafunzo yake mara kwa mara kwenda kwenye vyuo mbalimbali vya Wizara ya Maliasili na utalii nchini, chuo kina umuhimu mkubwa kutokana na kuwa ni chuo pekee katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Siku za nyuma chuo kiliweza kupata watu kutoka nchi za nje kuja kujifunza, hivyo serikali haiwezi kukiacha solemba! Kama tumeweza kujenga Chuo kikubwa cha Serikali za Mitaa, Hombolo kinachotufanya tushindwe kujenga chuo kikubwa hivi ni nini? Kwamba hatuoni thamani yake? Si kweli, miaka kumi ijayo thamani yake itaonekana tu,” alisema Mhe. Waziri Mkuu.
Aliongeza kuwa, tatizo la kutoendelezwa kwa chuo hicho wakati mwingine kunatokana na viongozi kutojua kinachoendelea, hivyo aliomba uongozi kuwakilisha mpango mkakati wake ili serikali iweze kuipembua na kuona wapi pakuanzia.
Aidha, Mhe. Pinda aliipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa uamuzi wake wa kukirudisha Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki mkoani Tabora na kutoa onyo kwa yoyote atakayetaka kujaribu kukihamisha tena kutofanya hivyo ili serikali iweze kujipanga na kusonga mbele.
Aliongeza kuwa, Tanzania ina hifadhi za misitu na maji ya kutosha inayotoa fursa ya kuzalisha asali nyingi, hivyo amewaasa wananchi kuchangamkia fursa hiyo ili kuiwezesha nchi kushika namba moja kwa nchi za Bara la Afrika zinazozalisha asali.
“Tanzania hivi sasa inapitwa na Ethopia kwa uzalishaji asali, nchi ambayo haina misitu yakutosha, hili haliwezekani tuangalie mpango mikakati yetu. Ufugaji asali hauhitaji mtaji mkubwa, na soko lake ni la uhakika, tumshinde Ethiopia na hili linawezekana kama tutapanua mawazo yetu juu ya sekta hii,” alisema Mhe. Pinda.
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Khamis Kagasheki, alimshukuru Waziri Mkuu kwa moyo wake wakusimamia kidete sekta ya ufugaji nyuki nchini na kutoa fursa za ajira kwa wananchi wengi.
Aidha, Mhe. Pinda alisisitiza kiu yake ya kuona Tanzania inazalisa asali nyingi kwa kuwaahidi wahitimu kuwapa zawadi ya mizinga 100 endapo wataunga na kuunda kikundi cha ufugaji nyuki na kutumia elimu waliopata kuweza kujipatia kipato.
Katika kusisitiza hilo Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Bi. Fatma Mwasa naye aliwahidi wahitimu ambao ni wakazi wa mkoa wake, kuunda vikundi vya watu waiopungua kumi kwa kikundi ili aweze kuwapatia mtaji wa mizinga.
0 comments:
Post a Comment