Jaji Mutungi: Subirini mwone utendaji wangu - Sema Naye
Headlines News :
Home » » Jaji Mutungi: Subirini mwone utendaji wangu

Jaji Mutungi: Subirini mwone utendaji wangu

Written By Sema Naye - Naipenda Tanzania on Sunday, August 11, 2013 | 1:29 PM

Awataka Watanzania kuwa na subira wakati huu ambapo bado hajakabidhiwa rasmi ofisi na kuahidi kuwa  mtumishi wa watu wote pale atakapoanza rasmi majukumu aliyokabidhiwa.

 
Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman akimpongeza Francis Mutungi baada ya kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Jaji wa Mahakama Kuu katika hafla iliyofanyika Ikulu, Juni 19,2012. Jaji Mutungi jana aliteuliwa kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa. Picha na Maktaba.

Dodoma. Msajili mteule wa Vyama vya Siasa nchini,  Jaji Francis Mutungi amewataka Watanzania kutulia na kusubiri utendaji wake atakapokabidhiwa rasmi jukumu hilo jipya alilopewa na Rais Jakaya Kikwete.

Mutungi aliteuliwa kushika wadhifa wa msajili wa vyama vya siasa kuchukua nafasi ya John Tendwa ambaye amestaafu. Tendwa aliiongoza taasisi hiyo kwa miaka 13.

Mutungi alisema: “Ninafahamu nina majukumu mazito mbele yangu, lakini siwezi kusema chochote kwa kuwa sijakabidhiwa rasmi ofisi. Ninachotaka kusema ni kwamba nitakuwa mtumishi wa kila mmoja.”

Alikataa kusema kuwa akianza kuzungumza mambo mengi kwa sasa wakati hajaingia rasmi kazini haitakuwa na maana yoyote na badala yake ataonekana kuwa anawahisha mambo.

Jana katika Mahakama Kuu ya Dodoma, ilikuwa tabu kumpata kiongozi huyo hali iliyoonyesha huenda alikuwa katika maandalizi ya kuweka mafaili yake katika hali nzuri kabla ya kuwaaga watumishi wenzake na kwenda kuanza majukumu mapya.

Wasaidizi wake wa karibu hawakuwa tayari kuelezea alikuwa na kazi gani hasa, lakini walimwambia mwandishi kuwa Jaji alikuwa na majukumu mengi kiasi cha kukosa nafasi ya kuzungumza na mtu.

Hata hivyo, alipompigia simu msajili huyo licha ya kukataa kuzungumza mambo mengi kuhusu nafasi yake hiyo mpya, lakini alionekana kuwa na ushirikiano wa kutosha na kuwataka wananchi wasubiri kitambo ili akabidhiwe. Juzi akizungumza na gazeti hili, Tendwa alikataa kumshauri Mutungi na kusema kuwa anaamini atafanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu kama ambavyo miongozo inavyotaka.

“Mutungi atafanya kazi kwa mujibu wa sheria na kama ataanza kubezwa na wanasiasa afahamu kuwa sasa ndiyo anafanya kazi sawasawa.

Mawakili wamlilia

Mawakili mbalimbali wameelezea kuridhishwa na uteuzi wa Jaji Mutungi kuwa msajili wa vyama  vya siasa, huku wakimmwagia sifa kuwa ni mtu sahihi katika wadhifa huo na kwamba ana uwezo.

Wakizungumza na Mwananchi jana kwa nyakati tofauti, mawakili hao walisema Jaji Mutungi anafaa katika nafasi hiyo kulingana na sifa yake ya ujaji na uzoefu wa kisheria na kwamba wana imani kuwa ataiongoza vyema ofisi hiyo.

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (Tanganyika Law Society- TLS), Francis Stolla na mawakili Richard Rweyongeza na  Jerome Msemwa, walimzungumzia Jaji Mutungi.

Wakili Stolla alisema kuwa Jaji Mutungi ana uzoefu na amebobea katika sheria kuwa amekuwa katika mfumo wa Mahakama kwa muda mrefu tangu akiwa hakimu na akapanda hadi kufikia nafasi ya ujaji.

Alisema kwa muda wote huo ambao Jaji Mutungi amefanya kazi katika mhimili huo wa Mahakama tangu akiwa hakimu, Msajili Mahakama Kuu, Msajili wa Mahakama ya Rufani hadi kuteuliwa kwa Jaji hawajawahi kupata shaka kuhusu umahiri wake .

 Wakili Rweyongeza alisema Jaji Mutungi ni mtu sahihi katika nafasi hiyo.
Share this article :

0 comments:

 
Support : 255-272-545-994 | Jasper A.K. | Mas Template
Copyright © 2011. Sema Naye - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger