Rais wa Zanzibar aunda upya Baraza la Mawaziri
Written By Sema Naye - Naipenda Tanzania on Wednesday, August 21, 2013 | 1:52 PM
Aiondoa Wizara ya Fedha ofisini kwake, ateua baadhi ya mawaziri na makatibu wakuu wapya.
Zanzibar. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein amefanya mabadiliko ya shughuli za Serikali katika wizara mbalimbali na kuunda wizara mpya nne na kujiondoa katika usimamizi wa Wizara ya Fedha.
Rais Shein alirithi kutoka kwa Rais aliyemtangulia Amani Abeid Karume kwa Wizara ya Fedha kuwa chini ya Ofisi ya Rais, lakini sasa ameiachia na kuunda Wizara ya Fedha inayojitegemea baada ya kutokuwapo Zanzibar kwa kipindi kirefu.
Hata hivyo, katika mabadiliko hayo Rais Shein amejipa majukumu mapya kwa shughuli za kazi na utumishi kuwa chini ya ofisi yake tofauti na ilivyokuwa kabla ambapo ilikuwa ni wizara inayojitegemea.
Taarifa ya Ikulu ya Zanzibar iliyotolewa jana mjini hapa na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Abdulhamid Yahya Mzee ilisema Rais kwa kutumia kifungu cha 53 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 amebadilisha na kuhamisha baadhi ya majukumu katika wizara.
Taarifa ilisema kutokana na marekebisho hayo, zimeundwa wizara mpya nne ambazo ni Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalumu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Ofisi ya Rais, Kazi na Utumishi wa Umma, Wizara ya Fedha na Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto. Katika mabadiliko hayo Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi itakuwa chini ya Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora, Dk Mwinyihaji Makame, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora, Salum Maulid Salum na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora, Said Abdalla Natepe.
Katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalumu za SMZ itakuwa chini ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalumu za SMZ , Haji Omar Kheir, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ, Joseph Abdalla Meza, Naibu Katibu Mkuu (Tawala za Mikoa), Mwinyiussi A. Hassan na Naibu Katibu Mkuu (Idara Maalumu za SMZ), Julius Nalimy Maziku.
Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma itakuwa chini ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma, Haroun Ali Suleiman, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma, Fatma Gharib Bilal, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma, Yakout Hassan Yakout.
Wizara ya Fedha itaongozwa na Waziri wa Fedha, Omar Yussuf Mzee, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Khamis Mussa Omar na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Juma Ameir Hafidh.
Katika Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto itakuwa chini ya Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Zainab, Omar Mohamed, Katibu Mkuu Asha Ali Abdalla, Naibu Katibu Mkuu (Uwezeshaji na Ushirika), Ali Khamis Juma na Naibu Katibu Mkuu (Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto), Msham Abdalla Khamis.
Taarifa ilisema shughuli za Tawala za Mikoa na Idara Maalumu za SMZ zimeondolewa katika Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na kuundiwa wizara mpya, shughuli za Utawala Bora zimeondolewa kutoka Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora na kuhamishiwa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Pia katika mabadiliko hayo shughuli za Kazi zimeunganishwa na shughuli za utumishi na kuundiwa wizara mpya, shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi na ushirika zimeondolewa kutoka Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika na kuunganishwa na shughuli za Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto.
Vilevile shughuli za Tume ya Mipango zimeondolewa kutoka Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo na kuhamishiwa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Idara ya Uratibu na Shughuli za SMZ, Dar es Salaam imeondolewa kutoka Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo na kuhamishiwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment