MABASI maalumu kwa ajili ya kubeba wanawake yaja.
Written By Sema Naye - Naipenda Tanzania on Sunday, August 25, 2013 | 10:34 PM
Shiraz Rashid wa Kampuni ya Africarriers akimpa ufunguo ya mfano Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simon Group inayoendesha UDA, Robert Kisena (kushoto) ikiwa ni ishara ya kukabidhi mabasi 40 ya UDA, jana. (Na Mpigapicha Wetu).
MABASI maalumu kwa ajili ya kubeba wanawake, watoto na watu wenye mahitaji maalumu, yanatarajiwa kuanza kufanya kazi jijini Dar es Salaam, ikiwa ni hatua ya kukabili tatizo la usafiri kwa kundi hilo.
Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam (UDA) litaagiza mabasi 2,000 kwa ajili ya kutekeleza mpango huo mwakani.
Mwenyekiti Mtendaji wa Simon Group inayoendesha UDA, Robert Kisena alisema katika mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake, Dar es Salaam.
Alisema magari yatakayoagizwa ambayo ifikapo Juni mwakani yatakuwa yamefikishwa nchini, yanakidhi baadhi ya vigezo vya mabasi yaendayo haraka. Vigezo hivyo ni pamoja na kuwa na milango miwili na upana unaotakiwa.
Hivi karibuni, Wakala wa Usafiri wa Haraka (DART) ulieleza kuwa, awamu ya kwanza ya mradi wa mabasi yaendayo haraka utaanza kutoa huduma ifikapo Julai 2015 na utayaondoa katika barabara husika daladala 1,600 na zitahamishiwa maeneo mengine.
UDA pia inajikita kutoa huduma katika maeneo yote ya Jiji. Kisena alikuwa akizungumzia mipango ya muda mfupi na mrefu ya shirika katika kukabili adha ya usafiri, sanjari na uzinduzi wa mabasi mapya 40 ya abiria, yanayoanza kazi leo jijini humo.
Alisema, “Tunashirikiana na kampuni ya kutengeneza mabasi hayo iitwayo Eicher na wakala wake hapa nchini ni Africarriers hivyo tumedhamiria kuondoa adha ya usafiri Dar es Salaam na maeneo ya pembezoni mwa Jiji hili, tuna malengo ya muda mrefu ambayo hadi kufikia mwaka 2017, tutaingiza mabasi 5,000, utekelezaji wake umeanza.”
“Leo (jana) tunaingiza mabasi 40 ambayo yataanza kazi kesho (leo), haya hayahusiki na mabasi 2,000 ambayo hadi kufikia Juni mwakani, yatakuwa tayari kazini, kwa kuwa katika kupigania usafiri wanaoumia na kuteseka zaidi wanawake na watoto, tutakuwa na mabasi maalumu kwa ajili ya wanawake, watoto na watu wenye mahitaji maalumu,” alisema Kisena.
Kisena alisema wanawake wataruhusiwa kupakia mabasi ya watu wote yatakayokuwa yakitoa huduma katika maeneo yote jijini.
Lakini, wanaume hawataruhusiwa kupanda mabasi maalumu ya wanawake ili kutoa nafasi kwa akina mama, watoto na watu wenye mahitaji wakiwemo walemavu, kupata usafiri bila usumbufu wanaokumbana nao sasa.
Kisena alisema mabasi hayo yanagharimu takribani Sh bilioni 200 na kutakuwa na vituo saba pembezoni mwa jiji na kituo kimoja kikubwa kuwezesha wasafiri kupata huduma kwa wakati.
Alisema ili kufanikisha hilo, wanatarajia kumaliza kulipa deni lote la Sh bilioni 17 ambalo shirika linalodaiwa kabla ya Juni mwakani.
Ajira zaja Miongoni mwa utekelezaji wa mipango ya muda mfupi aliyoeleza Kisena ni pamoja na kuingiza katika usafirishaji mabasi 30 na jana mabasi 40 huku akieleza kuwa Oktoba mwaka huu, wataingiza mabasi mengine 100 nje ya mradi wa mabasi 2,000.
Alisema kupitia mradi huo, zaidi ya ajira 8,000 zitapatikana kutokana na basi moja kuhudumiwa na watu wanne. Pia alisema pamoja na kwamba mabasi ya Uda hayana mistari ya kuonesha njia, watayaweka alama maalumu ili abiria waweze kutofautisha.
Alisema hawatapandisha nauli ovyo ovyo hata kama mafuta yakipanda. “Tuna mbinu nyingi za kibiashara, hatutegemea kupandisha nauli ovyo ovyo, niwahakikishie wananchi hasa wakazi wa Dar es Salaam kuwa nauli zetu zitadumu kati ya miaka miwili hadi mitano, tuna mbinu nyingi za biashara kuwezesha hilo,” alijigamba Kisena.
Hisa za UDA Kuhusu hisa za UDA, alisema Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuuza hisa zake kwao ili kuliwezesha shirika kujiendesha kibiashara na kufikia malengo ya kuanza kupata faida katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Kwa sasa UDA ina umiliki wa wanahisa watatu ambao ni Simon Group yenye hisa milioni 8.9, serikali kuu yenye milioni 3.5 na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inayomiliki hisa milioni 3.6.
“Tunajua serikali haifanyi biashara, tunakusudia kutoa huduma bora kwa wananchi na ndio maana serikali ipo hatua za mwisho kuuza hisa zake kwetu, nimesikia pia kupitia vyombo vya habari kwamba Jiji nao wanauza hisa zao, hawajatuandikia rasmi nia yao hiyo lakini sisi tupo tayari kuzinunua, ila kama kuna Mtanzania mwenye uwezo wa kwenda sambamba na uwekezaji wetu, azinunue tu,” alibainisha Kisena.
Alisema serikali itabaki kwenye kukusanya kodi na kusimamia sheria kwa mujibu wa Sheria ya Uda ya Mwaka 1974. Alisema mpango wao ni kurejesha umiliki wa Uda kwa wananchi kwa kuiweka kwenye Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) kuwawezesha kununua hisa.
0 comments:
Post a Comment