Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bw. Ludovick S.L. Utouh amekutana na Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam ambapo ametoa ufafanuzi kukanusha tuhuma zilizotolewa katika baadhi ya vyombo vya habari vikimnukuu Mbunge wa Kigoma Kaskazini Mhe. Zitto Zuberi Kabwe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya PAC kwamba, kuna ufisadi katika matumizi ya fedha zilozotolewa katika bajeti ya 2011/2012 kwa ajili ya mradi maalum wa barabara unaosimamiwa na Wizara ya Ujenzi.
Bw. Utouh amebainisha kwamba kiasi cha Shs. 252,975,000 kilichohojiwa na ukaguzi ni fedha ambazo zimeonyeshwa kwenye taarifa za hesabu za Wizara kama ni miradi mipya ya mwaka 2011/2012 tofauti na uhalisia wenyewe ulivyo.
Serikali katika dhamira ya kuimarisha mtandao wa barabara nchini, iliweka kwenye bajeti yake ya mwaka wa fedha 2011/12 Kasma maalum ya ujenzi wa miradi ya barabara na kuitengea jumla ya shilingi 252,975,000,000.00 kwa ajili ya kulipia kazi za barabara zinazoendelea.
Fedha zote zilitolewa na HAZINA kwa madhumuni hayo na kwa kufuata taratibu za Serikali. Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS ililipia kazi hizo za barabara kwa maana ya madai ya Wakandarasi na Wahandisi Washauri wa miradi mbalimbali inayoendelea.
"Hivyo katika kujadili hesabu za Wizara ya Ujenzi hakukuwepo na tuhuma zozote za ufisadi ila Kamati ilimtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuihakikishia matumizi ya fedha hizo jambo ambalo litafanyika" alielezea Bw. Utouh.
CAG katika hatua nyingine alichukua fursa hiyo kuipongeza Wizara ya Ujenzi kwamba inafanya kazi nzuri sana ya kusimamia na kujenga barabara katika kona zote za nchi yetu. “Tuwapongeze kwa kazi nzuri wanayoifanya ili wawe na moyo wa kuchapakazi zaidi kwa maendeleo ya nchi yetu” alisistiza Bw. Utouh.
0 comments:
Post a Comment