Mazishi ya Meja Khatib Shaban Mshindo Kijiji kwao Fujoni Unguja.
Written By Sema Naye - Naipenda Tanzania on Monday, September 2, 2013 | 5:07 PM
Na Othman Khamis Ame
Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ } Meja Khatibu Shaaban Mshindo aliyefariki Dunia akiwa katika shughuli za ulinzi wa amani katika kikosi cha umoja wa Mataifa kwenye jimbo la Goma Nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo amezikwa kwa heshima zote za Kijeshi.
Wapiganaji wa Jeshi la Wananachi wa Tanzania { JWTZ } wakitoa salamu zao za mwisho wakati wa mazishi ya kamanda wao Meja Khatibu Shaaban Mshindo yaliyofanyika kijijini kwake Mangapwani.
Meja Shaaban ambaye alijeruhiwa vibaya kwa bomu katika eneo lake la kazi na kusababisha kuvuja damu nyingi na hatimae kusababisha kifo chake akiwa njiani kupelekwa Hospitali alizikwa kijiji kwao Mangapwani Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa Kaskazini Unguja.
Makamanda na wapiganaji wa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania , askari wengine wa vikosi vya ulinzi, wananchi , ndugu wa marehemu walishiriki kwenye mazishi hayo wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mohammed Aboud Mohammed.
Marehemu Meja Khatib Shaaban Mshindo alizaliwa Tarehe 29 Septemba 1972 katika Mtaa wa Rahaleo Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi na baadaye kupata elimu yake ya msingi na kuhitimu mwaka 1986.
Alijiunga na Skuli ya Sekondari uchama na kuhitimu kidato cha Nne mwaka 1990 ambapo baadaye akajiunga na kidato cha tano na sita katika skuli ya sekondari ya Alharamain na kumaliza mwaka 1993.
Meja Khatib Shaaban Mshindo alijiunga na Jeshi la wananchi wa Tanzania { JWTZ } Tarehe 1 machi 1995 na kutunukiwa heshima ya kamisheni tarehe 17 mei 1997.
Katika utumishi wake Meja Khatib Shaaban Mshindo alibahatika kuhudhuria mafunzo ya afisa mwanafunzi chuoni Monduli, kozi ya uongozi wa platuni, uongozi wa kombania pamoja na mafunzo ya operesheni Nchini Canada mwaka 2008.
Kamanda Khatib kutokana na ukakamavu wake alipandishwa vyeo kuanzia nafasi ya Luteni mwaka 1998, kepteni mwaka 2004 na kufikia cheo cha meja mwaka 2010 wadhifa aliokuwa nao hadi kufariki kwake.
Marehemu Meja Khatibu Shaaban Mshindo aliwahi kushika madaraka ya Kamanda wa Kikosi mwaka 1997, Mkufunzi kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2006 pamoja na kuwa kamanda wa kombania Mkoani Kibaha.
Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kutambua na kuthamini mchango wa Meja Khatibu Shaaban Mshindo alimtunuku nishani ya Miaka 40 ya JWTZ.
Umoja wa Mataifa katika mazishi hayo uliwakilishwa na Kamanda wa Vikosi vya Umoja huo Mjini Goma Nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo Meja D.B Samujeli .
Kamanda Khatibu Shaaban Mshindo aliyelitumikia jeshi la Wananchi wa Tanzania katika kipindi cha miaka 18 miezi saba na siku 28 ameacha kizuka mmoja na watoto watatu.
Mwenyezi Muungu alilaze roho ya marehemu Meja Khatibu Shaaban Mshindo mahali peMa peponi. Amin.
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment