

Profesa Muhongo akiangalia kipenyo cha bomba ambacho ni mita moja






Serikali yaridhishwa na kasi ya ujenzi wa bomba la gesi
Serikali imeridhishwa na kasi ya kazi inayofanywa ya mradi wa kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
Hayo yalibainika wakati Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Balozi wa China nchini, Lu-Youging walipofanya ziara ya pamoja kukagua ujenzi wa bomba hilo. Katika ziara hiyo walitembelea kambi tano za mradi za Somangafungu, Nyamwage, Ikwiriri, Mkuranga na Kongowe katika Mto Mzinga.
Waziri Muhongo alisema ameridhishwa na kasi ya kazi inayofanywa ya mradi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam huku akiwataka watanzania kuwa na imani na kazi hiyo.
Alisema awali zoezi hilo lilitakiwa kukamilika mwezi Januari, 2015, lakini huenda likawahi kumalizika kutokana na kuwepo kwa vifaa vya kisasa na imara kutoka Kampuni ya China Petroleum Pipeline (CPP) watakao fanya kazi ya kulitandaza.
Alisema mabomba hayo ni imara na yanaweza kudumu kwa zaidi ya miaka 70 iwapo yatatunzwa vizuri na kwamba serikali itahakikisha inayafuatilia vizuri na kuhakikisha hayachafuki
Waziri Muhongo alisema kazi ya kuunganisha vipande vya bomba inaanza rasmi tarehe 26 Agosti na wakati huo uchimbaji ukiendelea kwa ajili ya kuweka mabomba hayo ambayo yatakuwa tayari yameunganishwa.
“Uunganishwaji unafanywa na mitambo ya kisasa kabisa na hapo bomba linapochimbiwa ndio hapohapo uunganishaji unafanyika na bomba zitakazolazwa baharini zitaunganishwa hukohuko” alisema.
Alisema kwa bomba zitakazoenda baharini uzito wake ni mkubwa zaidi ikilinganishwa na bomba zitazotumika nchi kavu kwakuwa zitakazolazwa baharini zitawekewa zege maalumu.
“Bomba zitakazoenda baharini zitakuwa na uzito wa zaidi ya tani 10 baada ya kuwekewa zege ambapo kwa sasa zina uzito wa tani tatu” alisema.
Alisema kazi ya kutandaza mabomba baharini itaanza Septemba 16, mwaka huu kwa kuwa kazi hiyo inahitaji umakini mkubwa.
Profesa muhongo alisema pindi bomba hilo litapokamilika uzalishaji wa umeme utaongezeka kutoka megawati 1500 zilizopo hadi kufikia megawati 3000 mwaka 2015 na kuanza kuuza umeme utakaokuwa wa ziada kwa nchi jirani.
Kuhusu suala la ajira, Waziri alisema mradi huo tayari umezalisha ajira. Alisema magari ya watanzania yapatayo 45 yamepewa kazi ya kusafirisha mabomba huku watanzania wengine wakiajiriwa katika kazi zinazoendelea.
Balozi wa China nchini, Lu Youging alisema mradi huo ni wa kipekee na una umuhimu mkubwa sana kwa uchumi wa Tanzania kwani kupitia mradi huo, Tanzania itaweza kuwa na viwanda vingi na kupelekea kuongezeka kwa ajira nchini.
Aliongeza kuwa mradi huo utasaidia katika utunzaji wa mazingira kwakuwa badala ya kuendelea kukata miti kwa ajili ya mkaa na kuni, watanzania watatumia gesi asilia kwa matumizi ya kupikia.
0 comments:
Post a Comment